TAARIFA YA MATOKEO YA MITIHANI YA TAIFA YA MWAKA 2019

UTANGULIZI

Ndugu Wanafunzi, 

Walimu, 

Wazazi, 

Wanahabari na Wananchi kwa ujumla  

Assalaamu alaykum, 

Leo tumekutana hapa kwa ajili ya kutoa taarifa ya Matokeo ya Mitihani ya Taifa ya mwaka 2019 kama ilivyo kawaida yetu kila mwaka.

Mitihani ya Taifa ya Darasa la Nne, Darasa la Sita na Kidato cha Pili hufanywa kwa lengo la kupima na hatimaye kujua kiasi cha Maarifa, Ujuzi na Muelekeo wa Wanafunzi walioupata katika kipidi chote cha kujifunza. 

Matokeo haya yatawasaidia Wanafunzi katika kuongeza bidii na ari ya kujifunza katika madarasa yanayofuata. Aidha mrejesho wa matokeo ya mitihani hii utawasaidia Walimu kuweza kuimarisha mbinu za kufundishia na kujifunzia kwa ajili ya kukuza uelewa wa Wanafunzi na hatimaye kuinua kiwango cha ufaulu na ubora wa elimu nchini.

Matokeo ya Mitihani hii pia yatatumika katika kuwapanga wanafunzi katika ngazi ya juu kutoka ngazi aliyopo sasa.

Ndugu Wanahabari na Wananchi kwa ujumla ufaulu wa jumla katika mitihani ya mwaka 2019 umepanda katika ngazi zote na idadi ya watahiniwa waliofaulu kwa Daraja A hadi C imeongezeka ikilinganishwa na mwaka 2018.

Aidha, hakuna kesi yoyote ya udanganyifu iliyobainika katika mitihani hiyo.

UANDIKISHAJI NA MAHUDHURIO

DARASA LA NNE

Jumla ya watahiniwa 55,631 waliandikishwa kufanya mtihani huo katika Skuli 432 kati ya hizo 283 ni za Serikali na 149 ni za Binafsi, kati yawanafunzi walioandikishwa Wanawake   ni 27,379 sawa na asilimia 49.2 na Wanaume ni 28,252 sawa na asilimia 50.8. Idadi hii imeongezeka kwa watahiniwa 7,652 sawa na asilimia 15.9 ikilinganishwa na watahiniwa 47,979 walioandikishwa kwa mwaka 2018.

Watahiniwa 52,307 sawa na asilimia 94.0 walifanya mtihani huo ambapo  wanawake ni 26,429 sawa na asilimia 50.5 na wanaume ni 25,875 sawa na asilimia 49.5. Aidha, jumla ya watahiniwa 3,324 sawa na asilimia 6.0 hawakufanya mtihani huo kutokana na utoro na ugonjwa.

MATOKEO

Matokeo yanaonesha kuwa jumla ya watahiniwa 42,110 sawa na asilimia 80.5 wataendelea na masomo ya Darasa la Tano mwaka 2020 wakiwemo wanawake 22,773 sawa na asilimia 43.5 na wanaume 19,337 sawa na asilimia 37.0.

Ufaulu huu umepanda kwa asilimia 10.1 ikilinganishwa na ufaulu wa asilimia 70.4 wa mwaka 2018. Aidha, matokeo yanaonesha kuwa ufaulu katika daraja A, B, na C umepanda kwa kuwa na asilimia 40.0 ikilinganishwa na asilimia 26.0 ya mwaka 2018.

DARASA LA SITA

Uandikishaji wa watahiniwa wa Mtihani wa Taifa wa Darasa la Sita ulifanyika katika Skuli 380, kati ya Skuli hizo, Skuli 273 ni za Serikali na 107 ni za Binafsi. Kuna ongezeko la Skuli 07 sawa na asilimia 1.8 ikilinganishwa na Skuli zilizoandikishwa mwaka 2018. Watahiniwa 32,308 waliandikishwa kufanya mtihani huo kati yao Wanawake ni 16,940 na asilimia 52.4 na Wanaume ni 15,368 sawa na asilimia 47.6. Idadi hii imepungua kwa watahiniwa 4,404 sawa na asilimia 12 ikilinganishwa na watahiniwa 34,444 walioandikishwa mwaka 2018. Watahiniwa 31,185 walifanya mtihani huo sawa na asilimia 96.5 ambapo wanawake ni 16,633 sawa na asilimia 53.3 na wanaume 14,552 sawa na asilimia 46.7. Aidha watahiniwa 1,123 sawa na asilimia 3.5 hawakufanya Mtihani huo kutokana na sababu mbali mbali zikiwemo utoro na ugonjwa.

MATOKEO   

Ufaulu unaonesha kuwa jumla ya watahiniwa 30,419 sawa na asilimia 97.5 kati ya 31,185 waliofanya mtihani huu wamefaulu kwa madaraja ya A, B, C na D na watahiniwa 766 sawa na asilimia 2.5 hawakufaulu.

Ufaulu huo umepanda kwa asilimia 1.2 ukilinganishwa na ufaulu wa asilimia 96.3 wa mwaka 2018.

Idadi ya watahiniwa waliofaulu ambao wenye sifa ya kuendelea na masomo ya Kidato cha kwanza katika madarasa ya Vipawa (194), Michepuo (1,508) na Sekondari za kawaida (28,717) imeongezeka kwa mwaka 2019. Aidha Ubora wa ufaulu unaonesha kuwa idadi ya watahiniwa waliofaulu kwa Daraja A, B na C umepanda kwa kuwa na asilimia 41.3 ikilinganishwa na asilimia

37.4 ya mwaka 2018.

KIDATO CHA PILI

Uandikishwaji wa watahiniwa wa Kidato cha Pili ulifanyika katika Skuli 277 kati ya skuli hizo, Skuli 213 ni za Serikali na 64 ni za Skuli Binafsi. Kuna ongezeko la Skuli 14 sawa na asilimia 05 ikilinganishwa na Skuli 272 za Kidato cha Pili za mwaka 2018.

Jumla ya watahiniwa 34,473 walioandikishwa kufanya mtihani huo kati yao wanawake ni 18,502 sawa na asilimia 53.7 na wanaume ni 15,971 sawa na asilimia 46.3. Idadi hii ni pungufu kwa watahiniwa 668 sawa na asilimia 4.2 ikilinganishwa na watahiniwa 34,846 walioandikishwa mwaka 2018.

MATOKEO

Jumla ya watahiniwa 24,946 sawa na asilimia 76.8 kati ya 32,476 waliofanya mtihani huu wamefaulu kwa madaraja ya A, B+,B, C na D na watahiniwa 5,600 sawa na asilimia 17.2 hawakufaulu.

Ufaulu huu umepanda kwa asilimia 3.5 ikilinganishwa na ufaulu wa asilimia 73.3 wa mwaka 2018, ambapo idadi ya watahiniwa waliopata daraja A, B+,B na C umeongezeka ikilinganishwa na mwaka 2018. 

WANAFUNZI WALIOFANYA VIZURI ZAIDI KITAIFA

Matokeo yanaonesha kuwa wanafunzi waliofanya vizuri zaidi Kitaifa kwa madarasa yote ya mitihani ni:- 

Zainab Hussein Kurwa kutoka Skuli ya Upendo (Darasa la Nne). 

 Ummu-Kulthum Juma Ali Skuli ya Miti Ulaya (Darasa la Sita).

 Amina Hassan Khatib kutoka Skuli ya Lumumba (Kidato cha Pili).

SKULI ZILIZOFANYA VIZURI ZAIDI

Skuli zilizofanya vizuri zaidi Kitaifa kwa Darasa la Nne ni Skuli ya Great vision na Upendo nursury & primary school.

Skuli zilizofanya vizuri zaidi Kitaifa kwa Darasa la Sita ni Skuli ya Feza na Evergreen.

Skuli zilizofanya vizuri zaidi Kitaifa kwa Kidato cha Pili ni Skuli ya

Lumumba na Utaani B.

UFAULU WA KIWILAYA  

Kwa Mtihani wa Darasa la Nne, Wilaya ya Magharibi “B’’ inaongoza katika ufaulu wa ujumla kwa kupata asilimia 90.5 ikifuatiwa na Wilaya ya Mjini yenye ufaulu wa asilimia 89.9. Aidha, Wilaya ya Mkoani ni ya mwisho kwa kupata asilimia 67.3.

Kwa Darasa la Sita, Wilaya zote zimefanya vizuri na ufaulu wao umepanda ambapo Wilaya ya Micheweni inaongoza kwa Skuli za Serikali kwa kufanya vizuri zaidi kwa kupata asilimia 98.9 ambapo Wilaya ya Kati ni ya mwisho yenye asilimia 94.8. 

Kwa upande wa Mtihani wa Kidato cha Pili, Wilaya zote zimefanya vizuri ambapo Wilaya ya Micheweni inaongoza kwa kupata asilimia 83.4 na Wilaya ya Kaskazini ‘B’, Wilaya ya Kati na Wilaya ya Kusini   zinaonekana kuwa ni za mwisho kwa kupata asilimia 62.2, 62.4 na 63.1.

MAELEKEZO

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali inawataka wanafunzi wote ambao hawakufanya Mitihani ya Darasa la Nne, Sita na Kidato cha Pili mwaka 2019 warudie kusoma katika madarasa hayo.

Aidha wanafunzi 766 wa Darasa la Sita na Wanfunzi 5,600 wa Kidato cha Pili ambao hawakufaulu mitihani yao ya mwaka 2019 watarudia kusoma madarasa hayo na kufanya mitihani mwaka 2020.

PONGEZI ZA WIZARA

Wizara ya Eilmu na Mafunzo ya Amali kwa dhati kabisa inawapongeza wanafunzi wote waliofaulu katika mitihani yao kwa kuweza kuendelea na masomo katika madarasa yanayofuata na wanaombwa kuongeza bidii ili waweze kukuza uwezo wao wa kitaaluma kwa ajili ya kupata ufaulu mzuri zaidi katika mitihani ijayo. Aidha Wizara inatoa pongezi kwa Walimu kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuwapatia wanafunzi taaluma na maadili mema mambo ambayo yatawasaidia wakati wa sasa na baadae.  Pia Wizara inaendelea kuwashukuru Wazazi na walezi wa wanafunzi kwa kuwasimamia, kuwalea, kuwaongoza na kuwapatia watoto wao huduma za lazima na ili waweze kumudu masomo yao.

Aidha Wizara inatoa shukurani kwa wale wote walioshiriki katika kufanikisha ufanyaji wa mitihani hii katika hatua zake zote. Tunawashukuru Baraza la Mitihani la Zanzibar, Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Madereva na Makonda, Wenye vyombo vya Usafiri, Vyombo vya Habari, Chuo cha Polisi Ziwani, Skuli ya Glorious, Walimu, Wazazi na Walezi na wote walioshiriki kwa njia moja au nyengine katika kulifanikisha zoezi hili.

KUANGALIA MATOKEO.

Ndugu wanafunzi, Walimu na Wananchi kwa ujumla, Wizara inapenda kutaarifu kwamba matokeo ya mitihani hii yanaonekana katika tovuti zifuatazo:

www.moez.go.tz  

www.bmz.go.tz

Facebook: Wizara ya Elimu Zanzibar.  

Ahsanteni kwa kunisikiliza.  

Riziki Pembe Juma (MBM),

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali

Zanzibar.